DIRA YETU AFRIKA

Tunafanikiwa kwa Kuwainua Wengine

USITUME CV YAKO KWA MUAJIRI KABLA HUJAZINGATIA HAYA

Naruida tena Usitume CV yako kabla hujazingatia haya yafuatayo. Wakati Fulani nilikua nahitaji vijana watatu kwa ajili ya kazi za graphics designing, marketing and secretary; hivyo nikatengeneza tangazo ambalo baada ya kulipakia kwenye mitandao lilisambaa sana kwenye majukwaa tofauti tofauti hasa mitandao ya kijamii. Ndani ya muda wa wiki moja nilikua nimepokea maombi na cv Zaidi ya 70 za vijana wa kike na wa kiume wakijaribu bahati yao katika mojawapo ya kazi hizo tatu. Wingi wa zile CV pamoja na makosa yaliyokuwemo kwenye zile CV vikanisukuma kuandika Makala hii.

Hata leo bado nikiwa idara ya rasilimali watu katika tasnia ya hoteli na utaliii naendelea kupokea CV kila kukicha. Bado makosa kwenye CV zilizo nyingi yanafanana tena hasa kwa wale wanaoambiwa watume CV kupitia email. Tuendelee na mada husika ambayo inasema usitume cv kwa muajiri kabla hujazingatia haya na hii ni hasa kwa wale wanaotuma cv kupitia email.

Tambua vigezo vinavyohitajika kwenye kazi husika kabla ya kutuma CV

Sio kila tangazo la kazi linahitajia wewe utume maombi.  Matangazo ya kazi mengine lazima uyaache yakupite. Kuna watu wao kila akisikia tangazo la kazi na akaambiwa atume cv basi moja kwa moja anakimbilia kuchukua cv aliyoiandaa miaka kadhaa iliyopita na kuituma hivyo hivyo. Mbaya zaidi mwingine anaifowadi CV ambayo alishawahi kuituma kwa muajiri mwingine kabla. Hayo ni makosa makubwa sana. Kabla hujatuma cv tambua vigezo vinavyohitajika na maelezo ya kina kwenye kazi husika ndio uamue kuanza kuhuisha cv yako ama kuachana na hilo tangazo la kazi. Matangazo ya kazi mengine yanahitaji akina dada peke yao ndio watume CV unakuta na kina baba kibao nao wamefowadi cv zao mbovu.

Ipitie upya CV yako na fanya marekebisho yote muhimu

Ukijua vigezo na maelezo ya kina kuhusu tangazo la kazi utakuwa katika nafasi nzuri ya kuamua lipi la kufanya. Kama utaamua kutuma maombi ya kazi husika basi lazima upitie hatua hii ya kuipitia cv yako na kuihuisha. Kuhuisha cv ni mchakato wa kufanya marekebisho muhimu kama vile ujuzi wako, elimu yako pamoja na muda wa uzoefu katika sekta hiyo  ili CV yako iendane na vigezo vya kazi husika ikiwa ni pamoja na kurekebisha makosa ya kiundishi.

Jina gani la kuandika kwenye dokumenti ya CV ukisevu kwenye kompyuta?

Sasa tuseme tayari umemaliza kuiandaa vizuri CV yako na ina kila kigezo cha kumfanya mwajiri ainue simu yake na kukupigia hatua inayofuata ni ipi? Hapa sasa ndio ule muda wengi wetu tunafanya makosa madogo lakini yenye madhara makubwa mno. Wengi wetu tumesevu CV zetu kwenye kompyuta zikiwa na majina kama vile cv. New cv, Nasra cv 2, cv pdf . Usipokuwa makini katika kusevu jina mahususi la dokumenti yako ya cv ujue kuwa cv yako itaishia kwenye dustbin ya kompyuta wakati mwingine hata ikiwa haijasomwa na mwajiri. Kumbuka mwajiri anapokea cv tele kila siku cv zenye mashiko na nyinginezo ni takataka zote zikigombea nafasi ya kuonekana machoni mwa mwajiri ili afanye maamuzi ya kukupigia simu. Jingine na muhimu kabisa lazima CV yako iwe katika mfumo wa pdf. Kama nilivyokwisha kusema mwanzoni usifowadi cv uliyoituma kwa mwajiri A na ukafowadi tena kwa mwajiri B. Ipitie upya fanya marekebisho kisha fuata utaratibu ufuatao kusevu jina linalofaa kwenye kompyuta yako.

 Wewe ni Nani? Unaweza Kufanya nini? Una Uzoefu wa muda gani?

Nikiwa na uzoefua wa zaidi ya miaka 15 kwenye uajiri nakushauri utumie utaratibu huu kuipa jina CV yako kabla hujaituma. Jina la dokumenti ya CV yako iwe na angalau vipengele vitatu ambavyo ni Jina lako, Kazi unayoomba, na uzoefu wako. Mfano: Nkosi Wa Afrika Marketing PR 3 Years Experience. Katika CV zaidi ya 50 atakazopokea jina la hii CV tu litamvutia awe na shauku ya kuisoma kuliko zile zenye majina kama cv, au cv mpya. Kwanini? Hii ni kwa sababu ina jina la mwenye CV ambaye ni NKOSI WA AFRIKA, pia kuna Kitengo anachoombea kazi ambacho ni Marketing and Public Relations na pia imeonyesha kuwa huyu NKOSI WA AFRIKA anayetuma hii CV ana uzoefu wa miaka 3 mitatu. Huoni kama hii ni sababu tosha ya kuwashinda wale wengine wenye majina ya ajabu katika dokumenti za CV zao? Kumbuka lazima CV yako iwe katika mfumo wa pdf.

Ikiwezekana Kabla hujaituma hiyo CV yako mpe mtu mwingine nae aipitie atoe maoni yake.

Ukivaa vizuri ukapendeza labda gauni lako pendwa ama suruali yako ya mtoko unaweza ukasahau kufunga zipu. Kwa bahati mbaya anayeweza kuona vizuri kuwa hukufunga zipu ya nguo yako mara nyingi ni mtu mwingine anayekutazama na sio wewe mwenyewe. Hata kwenye uandishi pia ni hivyo hivyo kila kitu kinaweza kikawa sawa sawia kwenye CV yako. Lakini kumbe kwa bahati mbaya kukuwa na makosa madogo madogo pengine ya kiuandishi ambayo wewe hukuyaona lakini ukitumia busara kumpa mtu mwingine aipitie CV yako labda anaweza kuyaona. Fanya ivo.  Wakati mwingine tutazungumzia matumizi ya email, jinsi ya kuandika email ya kikazi. Nakukumbusha tu kuwa neno langu sio sheria sipo hapa kukushurtisha ufuate mtazamo wangu,  Waweza kufanya vyovyote utakavyo lakini katika kila unachofanya jifunze kwa waliotangulia na wakafanikiwa. Tumia Akili yako na Fuata moyo wako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *